Makamu wa rais wa klabu ya Inter Milan Javier Zanetti, ameunga mkono harakati za kuajiriwa kwa aliyekua mtendaji mkuu wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus Beppe Marotta.
Marotta anakaribia kuajiriwa na klabu ya Inter Milan, baada ya kuachana na Juventus mwezi uliopita, huku ikiamniwa hatua ya kiongozi huyo kuelekea mjini Milan huenda zikazaa matunda ya kufanikisha mpango wa mafanikio klabuni hapo.
Zanetti amesema, suala la kuajiriwa kwa Marrota linapaswa kuheshimiwa, kwa sababu klabu yao inahitaji mtu kama huyo, ambaye ataweza kubadilisha sura ya klabu yao, ambayo iliwahi kutamba miaka ya nyuma nchini Italia na barani Ulaya kwa ujumla.
Amesema tayari ameshakutana Marrota mara kadhaa na kufanya mazungumzo, na dalili zinaonyesha wakati wowote wataanza kufanya naye kazi ya kuhakikisha mapinduzi ya soka yanatokea tena mjini Milan.
“Tumekutana na Marrota mara kadhaa, ameonyesha nia ya kufanya kazi na sisi, suala hilo haliwezi kulaziwa damu kwa sababu tunamuhitaji, ni wakati mrefu klabu yetu imedumaa katika kusaka mafanikio, unapokua na mtu kama Marrota, huna budi kujiamini wakati wote.” Alisema Zanneti alipohojiwa na kituo cha televisheni cha mjini MIlan
“Siku karibuni nilikua China kwa ajili ya kukutana na mmiliki wa Inter Milan, ameonyesha kufurahishwa sana na hatua ya kukaribia kumpata Marrota, amenihakikishia mtu huyu atakapojiunga nasi, atapatiwa kila kitu ili aweze kufanya kazi yake kwa urahisi.” Aliongoza Zanetti ambaye aliitumikia Inter Milan kama mchezaji kuanzia mwaka 1995-2015.
Marrota amekua sehemu kubwa ya mafanikio ya klabu ya Juventus FC ambayo kwa sasa inaendelea kushikilia rekodi ya kutwaa ubingwa wa Serie A mara saba mfululizo tangu msimu wa 2011-12.
Klabu ya Inter Milan kwa mara ya mwisho ilitwaa ubingwa wa ligi ya nchini Italia msimu wa 2010-11.