Umoja wa Afrika, Marekani, Ufaransa na jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika (ECOWAS) zimelaani mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea na kutaka Rais Conde aachiliwe huru mara moja. 

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres ametuma ujumbe wa twitter akisema anafuatilia kwa karibu kinachotokea Guinea na kusema na kulaani kuchukuliwa kwa serikali kwa nguvu ya bunduki.

Katika taarifa ya karibuni rais wa AU Felix Tshisekedi na rais wa tume ya AU Moussa Faki wameitisha mkutano wa dharura wa taasisi za umoja huo kuhusu usalama na Amani ili kutathmini hali nchini Guinea na kuchukua hatua zifaazo.

Hatima ya Rais wa Guinea Alpha Condé haijulikani wazi baada ya video ambayo haijathibitishwa kumuonyesha mikononi mwa wanajeshi, ambao walisema wamefanya mapinduzi.

Bado haijulikani ni nini kinatokea huko Conakry Guinea, lakini wanajeshi wanasema wamechukua udhibiti. Katika hotuba iliyoonyeshwa kwa njia ya televisheni, wanaume walio na sare za kijeshi, bendera ya Guinea ikiwa nyuma yao wamelihutubia taifa

Kamati ya Kitaifa ya upatanisho na maendeleo, inalaumu ufisadi uliokithiri, usimamizi mbaya na umasikini nchini Guinea kwa uamuzi wao wa kufanya mapinduzi na wanasema katiba imevunjwa na kwamba kutakuwa na mashauriano ya kuunda katiba mpya, inayowahusisha watu wote na wamedai serikali imevunjwa na kwamba mipaka ya ardhi itafungwa kwa wiki moja.