Hofu imetanda ikihofiwa Nahodha na Kiungo wa timu ya taifa ya Wales, Aaron Ramsey huenda akakosekana kwenye mchezo wao muhimu dhidi ya Croatia kutokana na kupatwa na majeraha.
Hiyo ni baada ya taarifa kuwa kiungo huyo anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa majuma matatu na hivyo kuukosa mchezo dhidi ya Croatia wa kuwania kufuzu michuano ya Euro 2024 utakaopigwa Oktoba 15, mwaka huu.
Juzi Ramsey mwenye umri wa miaka 32 aliumia goti la kulia alipokuwa kwenye mazoezi na klabu yake ya Cardiff City inayoshiriki Ligi ya Championship.
“Siku mbili zilizopita tukiwa mazoezini (Ramsey) aliumia na nilipokea ripoti ya kitabibu iliyosema hatapatikana uwanjani kwa majuma matatu,” alisema kocha wa Cardiff, Erol Bulut.
“Ni goti la kulia, lile lile ambalo aliwahi kufanyiwa upasuaji miaka mingi iliyopita. Natumai kwamba tunaweza kuwa naye baada ya mapumzko ya mechi za timu za taifa,” alisema.
Licha ya ushindi wa mabao 2-0 wa mechi yao ya mwisho dhidi ya Latvia huku Ramsey akifunga bao moja, bado Wales imesalia nafasi ya nne katika Kundi D kwa pointi saba sawa na Armenia, wakizidiwa na vinara Croatia wenye pointi 10 sawa na Uturuki inayoshika nafasi ya pili.
Wales inahitaji ushindi dhidi ya Croatia ʻisiyofungika’ ili kuibua matumaini ya kuwa miongoni mwa timu mbili za Kundi D zitakazokufuzu michuano hiyo itakayofanyika Ujerumani.
Lakini kukosekana kwa mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal, inatazamiwa kuwa pigo kubwa kwa timu hiyo kuelekea katika mechi hiyo.
“Juma lililopita nilipata jeraha kwenye mazoezi. Nitatafuta ushauri wa kitaalamu juu ya hatua zinazofuata maana nimedhamiria kurejea na kusaidia timu haraka niwezavyo,” aliandika Ramsey kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.