Kiungo kutoka nchini Wales Aaron Ramsey, ameendelea kuwaweka njia panda mashabiki wa klabu ya Arsenal, kufuatia sakata lake la kutaka kuondoka mwishoni mwa msimu huu.

Ramsey amesema bado hajafanya maamuzi ya kuendelea kubaki klabuni hapo ama kuondoka, lakini ataangalia mwishoni mwa msimu huu, ambapo anaamini majibu sahihi yatapatikana.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, anamalizia mkataba wa mwaka mmoja uliosalia klabuni hapo, na bado hajasaini mkataba mpya, hali ambayo inaendelea kuzusha hofu miongoni mwa mashabiki, ambao wanahusudu waendelee kuuona akisalia Emirates Stadium.

Tayari alikua ameshaanza mazungumzo ya kusaini mkataba mpya miezi kadhaa iliyopita, lakini baadae taarifa zilieleza kuwa, mazungumzo kati yake na uongozi wa The Gunners yalivunjika, kufuatia kukosa muelekeo wa makubaliano ya baadhi ya vifungu kwenye mkataba huo.

Endapo ataondoka mwishoni mwa msimu huu, Ramsey atakua mchezaji huru, na tayari klabu za Italia AC Milan, Juventus na Inter Milan zimeanza kuhusishwa katika kuiwania saini yake.

Akizungumza mara baada ya mchezo wa jana kati ya timu yake ya taifa ya Wales na Hispania, Ramesey  alisema: “ Ninaendelea vizuri na klabu yangu ya Arsenal, suala la mkataba mpya nimelipa kisogo kwa muda, lakini mwishoni mwa msimu huu nitaangalia kama nitakua na maamuzi sahihi ya kubaki ama kuondoka.”

“Kwa sasa kazi yangu ni kucheza soka na kuiwezesha Arsenal kufikia malengo yake msimu huu, ninaamini hatua hii itaniwezesha kufikiria jambo moja, na hilo la mkataba mpya litakua baadae.”

Taarifa zinaeleza kuwa meneja wa Arsenal Unai Emery ameshafikia maamuzi ya kumuachia Ramesey kuondoka mwishoni mwa msimu huu, baada ya kukataa kusaini mkataba mpya, ambao ungemuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni 110,000 kwa juma.

Dkt. Bashiru: Vyama vya siasa nchini havina nidhamu
Mbowe ajibu mapigo, adai Chadema ilishiriki msiba wa ajali ya MV. Nyerere