Mwenyekiti ya Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo ametoa maoni yake kuhusu hotuba ya rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein iliyosisitiza kuhusu marudio ya uchaguzi visiwani humo.

Akiongea na kituo cha runinga cha ITV leo, Bulembo amewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi na kujitokeza kushiriki uchaguzi wa marudio pindi tarehe ya uchaguzi itakapotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwani utakuwa uchaguzi huru na haki kama ulivyopita.

“Cha kwanza amani. Rais ameonesha kwamba nchi itabaki kuwa kama vilevile ilivyo… ndani ya miaka 52 tumeishi kwa amani. Hilo ndilo kubwa sana ambalo watu wanalitilia mashaka. Na kawahakikishia kwamba lazima uchaguzi utakaofanyika utakuwa huru na haki kama ule uchaguzi mwingine ulivyopita,” alisema Bulembo.

“Kwa hiyo hicho ndicho unaweza kukishika mkononi ni amani. Na uchaguzi unafanyika ili tupate uongozi halali ili tuendelee kuwa na amani,” aliongeza.

Aidha, Bulembo aliwataka watanzania kwa ujumla kufahamu kuwa uchaguzi wa Zanzibar utawahusu wote kwa kuwa utahusu Jamhuri ya Muungano. Lakini aliwataka wenye haki kikatiba na waliojiandisha kupiga kura visiwani humo kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe itakayotangazwa.

 

“Katiba yetu inaongelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wapo wenzetu wanadhani labda uchaguzi unahusiana na Zanzibar, hapana. Uchaguzi huu (wa marudio) unahusiana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Samatta Azawadiwa Kiwanja Na Fedha
ISIS watajwa shambulizi la kujitoa mhanga Liloua Wageni