Kiungo wa klabu ya Ajax Amsterdam Abdelhak Nouri amebainika kuwa na matatizo ya misuli ya kichwa pamoja na ubongo, baada ya kufanyiwa vipimo kufuatia ajali mbaya aliyoipata akiwa katika mchezo wa kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Werder Bremen mwishoni mwa juma lililopita.
Nouri aligongana na mchezaji wa Werder Bremen na kuanguka vibaya, hali ambayo ilizua taharuki kwa viongozi wa benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenzake wa Ajax Amsterdam.
Kitendo hicho kilisababisha, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20 kukimbizwa hospitali kwa usafiri wa helkopta, na kwa kipindi cha siku kadhaa alikua akifanyiwa vipimo kabla ya usiku wa kuamkia leo kubainika ana matatizo ya misuli ya kichwa na sehemu ya ubongo.
“Kuna nafasi finyu sana kwa Nouri kupona majeraha yake,” imeeleza taarifa ya klabu iliyochapishwa kwenye tovuti ya Ajax Amsterdam. “Na hii ilisababishwa na kuchelewa kuwekewa hewa ya Oksijeni mara tu, alipoanguka.”
Nouri anaejulikana kwa jina la utani la ‘Appie, msimu uliopita alikitumikia kikosi cha Ajax Amsterdam katika michezo 15 ya ligi ya Uholanzi, pamoja na michezo mitatu ya michuano ya Europa League na alibahatika kufunga katika mchezo dhidi ya Willem II waliokubali kufungwa mabao matano kwa sifuri huko KNVB-Beker.
Nouri ambaye ni raia wa Uholanzi, amekuzwa na kituo cha vijana cha Ajax Amsterdam tangu mwaka 2005 na alipandishwa katika kikosi cha wakubwa mwaka 2016.