Beki wa Mtibwa Sugar Abdi Banda amewaomba radhi wadau wa soka nchini Tanzania kufuatia kauli aliyoitoa dhidi ya wachezaji wa Simba SC.
Banda alitoa kauli ya kuwakejeli kwa wachezaji wa Simba SC, baada ya mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Manungu Complex Jumamosi (Januari 22) na timu hizo kwenda sare ya 0-0.
Beki huyo ambaye amewahi kucheza soka Afrika Kusini kabla ya kurejea nchini msimu huu 2021/22, ameomba radhi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.
“Tuanze wiki mpya yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Huenda niliwaudhi au kuwakera wengi kila mmoja kwa nafasi yake naomba mnisamehe sana”
“Kwenye mpira au kwenye mchezo wowote kuna maneno ya kejeli na dharau kwa mpinzani wako au hata mchezaji mwenzako lakini hamaanishi kuna uhasama kama wengi walivyopokea maneno yangu. Michezo ni furaha na ajira basi tusichukulie kila kitu personal/serious sana'”
“Naomba mnisamehe sana maana kila mtu ana upokeaji wake na tafsiri yake. Sikuwa na lengo la kumbagua Henock Inonga au wachezaji wengine wa Simba SC. Tusahau yaliyopita, tupo kwa ajili ya kujenga na kuutangaza mpira wetu na sio chuki wala ubaguzi wowote hasa kwa wachezaji wanaokuja kucheza hapa kwetu”