Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin amezungumzia uwezekano wa kutua Coastal Union msimu ujao baada ya timu hiyo kutangaza kuvunja benchi la ufundi chini ya Fikiri Elias.
Moallin amesema hawezi kuzungumza lolote juu ya hilo, hivyo muda ukifika ataweka wazi wapi atakwenda ingawa lengo ni kubaki Tanzania.
“Siwezi kusema taarifa hizo ni za kweli au la, kwa sababu sijasaini mkataba na timu yoyote. Ni kweli niko kwenye mazungumzo na baadhi ya klabu hivyo tusubiri,” amesema.
Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omary Ayoub amesema kuvunja benchi lote la ufundi wanataka kutengeneza imara zaidi ili kuepuka kucheza kwa presha kama msimu ulioisha.
“Mambo mazuri yanakuja hivyo mashabiki wasifadhaike na hiki ambacho tumekifanya. Tutaleta watu ambao tunaamini watakuwa na msaada mkubwa kwenye benchi pamoja na usajili wa nyota wapya,” amesema.
Moallin alitua nchini akiwa mkurugenzi wa Ufundi wa Azam kabla ya kupewa kibarua cha kuinoa timu ya wakubwa Januari mwaka jana akichukua nafasi ya George Lwandamina ambaye alitimuliwa.
Hata hivyo matokeo yasiyorishisha yaliwafanya viongozi wa Azam kumtimua Agosti, mwaka jana na timu kupewa Denis Lavagne ambaye hakudumu pia kutokana na kuanza msimu vibaya.