Uongozi wa Coastal Union umeonesha nia ya kufanya kazi na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin, baada ya kumpatia mkataba na ili aupitie kabla ya kutoa majibu na kuusaini ili kuchukua mikoba ya Fikiri Elias aliyeachwa.
Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo kimeeleza kuwa Moallin aliomba kwanza kupitia mkataba huo kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, huku akipewa kutoa majibu kabla ya keshokutwa Jumatano ya Julai 5.
“Tunaamini uwezo wa Moallin kutokana na falsafa zake hasa kwenye soka la vijana ambao tumekuwa tukiwatumia kwa wingi katika kikosi chetu, hivyo hatuna wasiwasi na uwezo wake,” kimesema chanzo hicho
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Coastal, Omary Ayoub amesema awali mapendekezo yao yalikuwa ni kwa makocha watatu lakini hadi sasa wamebaki wawili ambao wanaendelea kuwachambua.
“Mambo mazuri yanakuja zaidi kwa mashabiki wetu kuanzia benchi jipya la ufundi, wachezaji wapya ambao tunaamini wataleta manufaa kwenye kikosi chetu hivyo hakuna kitakachoharibika,” amesema.
Alipotafutwa Kocha Moallin ili kuzungumzia hilo, alisema bado ni mapema kuweka wazi juu ya kuhusishwa na Coastal, lakini kama dili lipo basi atafurahi kwani malengo yake ni kuendelea kubaki nchini.
Moallin mwenye asili ya Somalia alitua nchini akiwa mkurugenzi wa ufundi wa Azam FC kabla ya kupewa timu ya wakubwa Januari, mwaka jana akichukua nafasi ya Mzambia George Lwandamina aliyetimuliwa.
Hata hivyo matokeo yasiyorishisha yaliwafanya viongozi wa Azam FC kumtimua Agosti, mwaka jana na timu kupewa Mfaransa Denis Lavagne ambaye hakudumu pia kutokana na kuanza msimu vibaya.