Kocha Mkuu wa Azam FC Abdihamid Moallin amesema ameanza kupata picha ya kikosi alichokihitaji tangu alipokabidhiwa majukumu ya kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la klabu hiyo.
Jumatano (Machi 16), Azam FC ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Namungo FC na Jumamosi (Machi 19) iliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya timu ya Taifa ya Somalia katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Jijini Dar es salaam.
Kocha Moallin amesema sasa anaiona timu yake inaanza kuimarika katika ari na upambanaji kwa wachezaji wake kitu ambacho walikikosa kwenye michezo mitatu iliyopita.
“Hiki ndicho tulikuwa tunakikosa katika michezo tatu iliyopita, lakini tumethibitisha kuwa makini tukianzia kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC ugenini na sasa Somalia,” amesema Moallin.
“Mechi zote zilikuwa ngumu, lakini tumepigania alama tatu.“Sasa natarajia kuona michezo ijayo wachezaji wangu wanajitoa kupambana kutafuta alama muhimu.” amesema Kocha huyo kutoka Marekani mwenye asili ya Somalia.
Azam FC itacheza na Young Africans mapema mwezi April katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.