Kiungo Kutoa Visiwani Zanzibar Abdul Aziz Makame ‘BUI’ amethibitisha kupokea taarifa za kuvunjwa kwa Mkataba wake na Klabu ya Kagera Sugar ambayo ilimsajili mwanzoni mwa msimu huu 2022/23, akitokea Namungo FC.
Mapema leo Jumanne (April 04) Kagera Sugar ilithibitisha kuvunjwa kwa mkataba wa mchezaji huyo, ambaye anaondoka klabuni hapo baada ya kudumu kwa miezi minne tangu aliposajiliwa.
Makame amekiri kupokea taarifa hizo akiwa nyumbani kwao Visiwani Zanzibar na ameahidi kuanza maisha mapya ya kusaka mahala pengine pa kucheza soka lake kwa msimu ujao wa 2023/24.
“Nimepokea barua yao ya kuvunja mkataba hivyo kwa sasa nipo huru, ninajipanga na maisha mapya ya kutafuta klabu nyingine ya kuitumikia kw amsimu ujao wa Ligi Kuu, iwe huko Bara ama hapa Zanzibar, kwa sababu soka ni ajira yangu.” Amesema kiungo huyo
Sababu kubwa ambayo imefahamikwa kuwa chanzo cha nyota huyo kuachwa ni kutokana na kushindwa kuhudhuria kwenye kituo cha kazi kwa muda aliopangiwa akieleza anauguza goti Visiwani Zanzibar.
Hata hivyo, mbali na hilo inaelezwa Makame hana uhusiano mzuri na Maxime kwani mara kadhaa wamekuwa wakitofautiana mazoezini na kusababisha migogoro, hivyo viongozi wakaona ni vyema kuachana naye.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Kagera, Mecky Maxime amemtakia kila la kheri Abdul Aziz Makame, huku akikiria kumpoteza mchezo mwenye uwezo na kipaji cha hali ya juu.
“Ni mchezaji mzuri ambaye ana ushirikiano na wenzake ila sisi kama benchi la ufundi tunauheshimu uamuzi wake aliouchukua kwani ameona iwe hivyo na ni sahihi kwake, tunamtakia kila la kheri,” amesema Maxime Beki na Nahodha wa zamani wa Taifa Stars aliyeng’ara enzi zake akiwa Mtibwa Sugar. Abdul Aziz Makame amewahi kuzitumikia klabu za Young Africans na Namungo FC zote zinzshiriki Ligi Kuu Tanzania bara msimu huu 2022/23.