Hatimaye jibu la wapi atakapocheza Kiungo Mshambuliaji Abdul Seleman Sopu msimu ujao 2022/23 limepatikana, baada ya Azam FC kuthibitisha kuinasa saini yake.

Mapema leo Jumatatu (Julai 04), Sopu alitajwa kumalizana na Uongozi wa klabu hiyo, lakini kulikua hakuna uthibitisho wowote kutoka Azam FC, hivyo taarifa hizo ziliwekwa mitandao kama Tetesi.

Baadae mchana Azam FC walithibitisha kumalizana na Kiungo huyo ambaye alionesha uwezo mkubwa wakati wa mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kati ya Coastal Union dhidi ya Young Africans, akifunga mabao matatu pekee yake.

Azam FC wameweka picha za Sopu akisaini mkataba wa miaka mitatu, akiwa sambamba na Tajiri wa Klabu hiyo Yusuph Bakhresa pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu Abdul-Karim Amin ‘Popat’.

“Tunayo furaha kuwataarifu kuwa tumeingia mkataba wa miaka mitatu na kiungo mshambuliaji, Abdul Sopu, akitokea Coastal Union.” Imeeleza taarifa iliyoambatana na picha za Sopu akisaini mkataba wa Azam FC.

Inaelezwa kabla ya Fainali ya ASFC dhidi ya Young Africans, Sopu alisaini mkataba wa miaka miwili na Coastal kwa dau la milioni 30, hivyo kuondoka kwake klabuni hapo kumeilipa klabu hiyo ya jijini Tanga zaidi ya Shilingi million 70.

Kabla ya kuthibitika amesajiliwa Azam FC, klabu kongwe za Simba SC na Young Africans zilizo kwenye mawindo ya usajili katika kipindi hiki, zilitajwa kumuwania mchezaji huyo.

Ahmed Ally awatuliza mashabiki Simba SC
Simba SC yakubali yaishe, Morrison aondoke tu!