Mataifa kadhaa ya Umoja wa Ulaya tangu jana Jumapili yamekuwa yakipiga marufuku kuingia kwa ndege za abiria zinazotokea nchini Uingereza, ili kuzuia kuenea kwa aina mpya ya virusi vya Corona vilivyogunduliwa nchini humo.
Ujerumani pamoja na mataifa mengine kadhaa, yalianza kuchukua hatua hiyo baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kutangaza kuzuka kwa aina hiyo mpya na sugu ya virusi vya Corona, kusini mwa Uingereza.
Punde baada ya kutoa tangazo hilo, Boris alitangaza masharti magumu na kuwataka mamilioni ya wanachi wa eneo hilo kubakia majumbani, kwa sababu virusi hivyo vilianza kusambaa kwa kasi kubwa.
Wakati huo huo, Shirika la Dawa la Ulaya, linakutana leo kuidhinisha chanjo ya kwanza dhidi ya COVID-19 kwa mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya, chanjo itakayotolewa kwa mamilioni ya raia wa umoja huo.