Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic amekataa kuzungumzia mustakabali wake ndani ya kikosi cha Man Utd, baada ya Jose Mourinho kusisitiza suala la kutaka kuona akisaini mkataba mpya.
Zlatan aliwaambia waandishi wa habari, bado ni mapema kuzungumzia suala hilo kutokana na kutambua umuhimu wa mapambano yanayoikabili Man Utd hadi mwishoni mwa msimu huu.
Mshambuliaji huyo ambaye aliisaidia Man Utd kushinda mchezo wa fainali wa kombe la ligi nchini England (EFL Cup) siku ya jumapili, amekua katika sintofahamu kuhusu mustakabali wake, kutokana na mkataba wake wa mwaka mmoja kutarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.
Ibrahimovic mwenye umri wa miaka 35, alisema: “Acha tuangalie nini kitakachotokea. Bado tuna miezi miwili mbele kabla ya kuisha kwa mkataba wangu.”
“Kwa mujibu wa wadau wengi wa soka, ninapaswa kufanya jambo wanalolitarajia, lakini bado ninasisitiza muda ukifika jambo hili litafahamika.”
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Swedish, ameshaifungia Man Utd mabao 26, tangu alipotua Old Trafford mwanzoni mwa msimu huu akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Ufaransa PSG.