Wababe wa Stamford Bridge (Chelsea) huenda wakamkosa mshambuliaji kutoka nchini Argentina na klabu ya Juventus ya Italia Gonzalo Higuain, kufuatia uongozi wa AC Milan kuonyesha nia ya dhati kuhitaji huduma ya mchezaji huyo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Sky Italia, kiongozi wa Juventus Giuseppe Marotta ameanza kufanya mazungumzo na mkurugenzi wa michezo wa Inter Milan ili kukamilisha mpango wa usajili wa Gonzalo Higuain.
Taarifa zinaeleza kuwa wawili hao wameanza kufanya mazungumzo hayo tangu siku ya jumamosi na jana jumapili walionekana pamoja mjini Milan, jambo ambalo linadhihirisha kuna uwezekano mkubwa wa biashara ya usajili wa mshambuliaji huyo ikafanyika wakati wowote.
Chelsea walikua wanapewa nafasi kubwa ya kumsajili Higuain, kufuatia kuajiriwa kwa meneja mpya Maurizio Sarri, ambaye aliwahi kufanya kazi na mchezaji huyo alipokua SSC Napoli.
Hata hivyo mpaka sasa hakuna taarifa rasmi za makubalino baina ya klabu ya Juventus na AC Milan, zaidi ya kuripotiwa kwa mazungumzo ya pande hizo mbili.
Juventus wameamua kumuweka sokoni Higuain katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, baada ya kumsajili mshambuliaji Cristiano Ronaldo kutoka Real Madrid ya Hispania.