AC Milan wamerejea tena kutaka kumnunua kiungo wa kati wa Chelsea na England, Ruben Loftus-Cheek, vyanzo vimethibitisha kwa 90minutes.
Miamba hiyo ya Ligi Kuu Italia, Serie A, ambao wameidhinisha kuondoka kwa Sandro Tonali kwenda Newcastle United, wako sokoni kwa ajili ya kuimarisha safu ya kati huku wakipania kujiimarisha baada ya kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.
Kikosi hicho cha kocha Stefano Pioli kimekuwa kikijaribu kuweka makubaliano ya kumnunua David Frattesi wa Sassuolo, lakini wanakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani wao wa jiji moja Inter Milan, ambao wanatafuta kuchukua nafasi ya Marcelo Brozovic anayelengwa na Barcelona na Saudi Arabia.
Milan walikuwa wameanza mazungumzo na Chelsea Mei mwaka huu kuhusu mpango wa kumnunua Loftus-Cheek, lakini ‘Rossoneri’ hao wakamfukuza Mkurugenzi wa Ufundi, Paolo Maldini na Mkurugenzi wa Michezo, Ricky Massara, ambao ndio walikuwa wameanza mchakato wa kumtaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27.
Mazungumzo yameanza tena kati ya Milan na Chelsea, na pande hizo mbili zilizungumza mwishoni mwa juma ili kupanga jinsi ya kuendelea, walijadili pia upatikanaji wa Conor Gallagher, Christian Pulisic na Pierre- Emerick Aubameyang.
Chelsea imekuwa ikitafuta kupokea ada ya takriban pauni milioni 20 kwa Loftus-Cheek, lakini inaaminika kuwa Milan wanatarajia kufikia makubaliano yenye thamani isiyozidi pauni milioni 17.
Loftus-Cheek amebakiza miezi 12 tu kwenye mkataba wake msimu huu wa majira ya joto na tayari ameambiwa na Chelsea kwamba anaweza kuhama, Iwapo Loftus-Cheek ataondoka Chelsea msimu huu wa majira ya joto, ataungana na wachezaji wengi wanaoelekea kwenye mlango wa kutokea huku klabu hiyo ikijiandaa kuingia katika zama mpya chini ya kocha Mauricio Pochettino.
N’Golo Kante na Kalidou Koulibaly tayari wameondoka na kujiunga na Al Ittihad na Al Hilal, huku Edouard Mendy na Hakim Ziyech nao wakiwa njiani kuelekea Saudi Arabia kujiunga na Al Ahli na Al Nassr.