Mgodi wa dhahabu wa Acacia Bulyanhulu (BGML) uliopo Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga umekabidhi hundi yenye thamani ya Shilingi milioni 460,732,841.08/= kwa ajili ya ushuru wa Huduma kwa halmashauri ya Msalala.
Hundi hiyo imekabidhiwa na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Graham Crew ambapo amesema kuwa kiasi hicho ni asilimia 67 ya malipo ya ushuru wa huduma kwa ajili ya kipindi cha miezi sita kuanzia Januari hadi mwezi Juni mwaka huu ambacho ni asilimia 0.3 ya ukokotoaji wa ushuru wa huduma wa mgodi huo katika kipindi hicho.
Amesema kuwa Ushuru huo umepungua kwa kuwa mgodi haujafanya mauzo ya makinikia ambayo yamezuiliwa bandarini tangu mwanzoni mwa mwezi machi mwaka huu, hivyo ameahidi kulipa kiasi kikubwa zaidi pindi watakapouza makinikia yanayokusanywa mgodini.
“Jumla ya malipo ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha miezi sita iliyopita ni shilingi za Kitanzania 687,660,956.84/=,ambapo malipo hayo yamegawanywa katika halmashauri mbili ambazo ni Msalala inayopata asilimia 67 na Nyang’wale iliyopo mkoani Geita inapata asilimia 33,”amesema Crew.
Aidha, Katika hatua nyingine Crew amesema kuwa tangu mwaka 2000 mpaka sasa mgodi huo umelipa zaidi ya shilingi 10,247,742,957/= za kodi ya ushuru wa huduma na kampuni ya Acacia ilianza kutoa malipo ya ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 ya mapato ghafi kwa halmashauri husika mwaka 2014.
Hata hivyo, Akipokea hundi hiyo na kuikabidhi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Mkuu wa wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu ameushukuru mgodi wa Acacia Bulyanhulu kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutoa huduma kwa jami.