Hasira Hasara! Ndicho kilichotokea Ijumaa, Septemba 11, 2020, baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 29 kuchoma nyumba ya familia yake katika eneo la Kirinyaga nchini Kenya, kwa kile kinachoaminika kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kwa mujibu wa Citizen TV, mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina la Caroline Nyakio alitekeleza tukio hilo wakati mumewe James Mwagi akiwa ametoka.

Mwagi amesimulia kuwa kulikuwa na ugomvi mkubwa kati yao, lakini hakutarajia kuwa mkewe angefikia hatua ya kuchoma nyumba yao yenye thamani ya Sh. 750,000 za Kenya (Sawa Sh. 1 6 za Tanzania).

“Niliamua kutoka nyumbani nikaenda Kimunye Trade Center baada ya kutokea ugomvi mkubwa kati yangu na mke wangu Caroline Nyakio, alitolea maneno makali sana, lakini nilipata mshtuko mkubwa baada ya kupigiwa simu na majirani wakiniambia kuwa nyumba yetu ilikuwa inateketea kwa moto,” Mwangi ameiambia Citizen TV.

Ameongeza kuwa alifahamu mkewe ndiye aliyetekeleza tukio hilo baada ya kupata taarifa kwamba alinunua mafuta ya petrol na kuyapeleka katika nyumba hiyo. Hata hivyo, amesema hakuna mtu aliyejeruhiwa kutokana na tukio hilo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Gichugu, Anthony Mbogo amelaani kitendo hicho na kueleza kuwa wanamshikilia mtuhumiwa wakati uchunguzi ukiendelea.

Mali: Jeshi kuunda serikali ya mpito
NEC yawarejesha wagombea 24 wa udiwani kwenye uchaguzi