Klabu ya Borussia Dortmund imekamilisha usajili wa beki wa pembeni kutoka nchini Morocco, Achraf Hakimi akitokea kwa mabingwa wa soka barani Ulaya, Real Madrid.
Borussia Dortmund wamekamilisha dili hilo kwa makubaliano ya kumsajili Hakimi kwa mkopo wa miaka miwili.
Beki huyo ambaye ana sifa ya kupanda na kushuka anapokuwa uwanjani, atacheza ligi ya Ujerumani msimu ujao, huku akikumbukwa kwa mchango wake alioutoa akiwa na timu ya taifa ya Morocco katika fainali za kombe la dunia zitakazofikia tamati mwishoni mwa juma hili nchini Urusi, baada ya kucheza michezo mitatu ya hatua ya makundi.
Hakimi mwenye umri wa miaka 19, amekuzwa kwenye kituo cha vijana cha Real Madrid. Aliyekuwa meneja wa klabu hiyo, Zinedine Zidane alilazimika kumtumia katika kikosi cha wakubwa msimu uliopita katika michezo tisa ya ligi, michezo mitano ya kombe la mfalme na michezo miwili ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
“Achraf Hakimi ni mchezaji kinda, ana uwezo mkubwa wa kufanya lolote anapokuWa uwanjani hususan katika jukumu la kuzuia. Amecheza kwa mafanikio makubwa akiwa na Real Madrid pamoja na timu ya taifa ya Morocco,” alisema mkurugenzi wa michezo wa Dortmund Michael Zorc, baada ya kukamilisha usajili wake.
Hakimi anakuwa mchezaji wa sita kusajiliwa chini ya utawala wa meneja mpya klabuni hapo Lucien Favre, akitanguliwa na walinda milango Marwin Hitz na Eric Oelschlagel. Wengine waliotangulia ni viungo Thomas Delaney na Marius Wolf, pamoja na beki Abdou Diallo.
Anatarajiwa kujiunga rasmi na kikosi cha Dortmund mwanzoni mwa juma lijalo, tayari kwa ziara ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi ya nchini Ujerumani, watakayoifanya huko Marekani kauanzia Julai 18-26.