Klabu ya Real Madrid imehusishwa na mabeki wapya wa pembeni kutokana na uhaba wao wa sasa katika maeneo hayo, huku mhitimu wa akademi yao Achraf Hakimi akitajwa kuwa mbioni kurejea Santiago Bernabeu kutoka PSG.
Wakala wa Hakimi amekiri kuwa beki huyo wa kulia ana nia ya kurejea Real Madrid msimu huu wa majira ya joto.
Ingawa ni mchezaji wa Kimataifa wa Morocco, Hakimi alizaliwa na kukulia Madrid, akitokea katika safu ya vijana kule ‘Los Blancos’ na kucheza mara 17 kwenye kikosi cha kwanza.
Hakimi alijiunga na Borussia Dortmund kwa mkopo wa miaka miwili mwaka 2018 kabla ya kusaini Inter Milan kwa uhamisho wa kudumu.
Alijidhihirisha kuwa mmoja wa mabeki wa pembeni bora zaidi duniani, lakini akaondoka kwenda Paris Saint-Germain baada ya msimu mmoja tu pale San Siro kutokana na masuala ya kifedha ya ‘Nerazzurri’.
Akiwa PSG, Hakimi ameendelea kupaa na ni eneo la uwanja ambalo Real Madrid wamehangaika kulijaza katika misimu ya hivi karibuni.
Katika mahojiano na AS, wakala wa Hakimi, Alejandro Camano, alifungua mlango wa kurejea Santiago Bernabeu.
“Achraf amekuwa mbali na Real Madrid kwa miaka mitano, lakini huwa ni nyumbani kwake, mahali fulani moyoni mwake klabu iko pale,” alisema Camano.
“Kama Real Madrid wanataka kumsajili tutasikiliza, ukimuuliza utaona ni shabiki wa Real Madrid, lakini mradi wetu sasa ni wa PSG.
“Wachezaji wakuu siku zote wanaona Real Madrid kama shabaha. Ni wachezaji wangapi wangependa kwenda huko? Achraf aliishi hivyo, na ameundwa kwa maadili ya klabu.”