Boniface Gideon – Tanga.
Chama cha ACT-Wazalendo na wakazi wa jiji la Tanga wamejitokeza kuchangia Damu Salama kwaajili ya wagonjwa wanaopatiwa huduma kwenye Hospitali ya Rufani Mkoa – Bombo.
Uchangiaji huo wa Damu Salama umeenda sambamba na zoezi la uhamasishaji kwa jamii juu ya faida za uchangiaji wa Damu Salama ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani yanayofanyika kila Agosti 13.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake chama hicho Mkoa wa Tanga, Rehema Mohammed aliwaambia Waandidhi wa Habari kuwa Chama hicho kinatarajia kufanya kongamano la Vijana Agosti 13, ikiwa ni Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Amesema, ‘’kwa kuzingatia umuhimu wa Damu kwasisi wanawake chama chetu kimeona ni vyema kuokoa maisha ya watu wengine na tunaendelea kufanya hamasa hii kwa Wakazi wote wa Tanga kujitokeza kwa wingi kwenye uchangiaji wa Damu.”
Aidha, Rehema alisema kabla ya maadhimisho hayo wanatarajiwa kufanya matukio mbalimbali ikiwamo kufanya mikutano ya hadhara na makongamano yakuwaelimisha Vijana juu mambo mbalimbali ya nchi yao ikiwamo uzalendo kwa Taifa.