Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Sendwe Mbaruku ametangaza kuaghirisha mkutano wao uliotakiwa kufanyika siku ya leo, Aprili 22, 2018 katika ofisi ya Chama Mkoa wa Kigoma mpaka pale utakapotangazwa tena.
”Ndugu wananchi wa Mkoa wa Kigoma, Mkutano wa ndani wa Mbunge Zitto Kabwe uliokuwa ufanyike leo mchana, ofisi za ACT Wazalendo mkoa kuzungumzia changamoto zetu umeaghirishwa mpaka utakapotangazwa tena”.
Taarifa hiyo imetolewa kupitia kurasa wa Twitter wa chama hicho na kudai kuwa imeamua kusitisha mkutano huo kwa sababu za kiusalama.
”Sababu za kuaghirishwa ni suala la usalama wa Zitto Kabwe, baada ya tishio dhidi ya maisha yake. Kamati ya ulinzi na usalama Taifa ya chama imetushauri tuchukue hatua hii. Tunawaomba radhi, tutawajulisha tarehe ya Mkutano wetu”
Aidha mkutano huo wa ndani wa mbunge wa Kigoma Mjini ulilenga kufanya mjadala juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Changamoto za kupata vitambulisho vya uraia vya NIDA kwa wenyeji wa mkoa wa Kigoma, Hati ya ukaguzi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hoja za Ukaguzi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Miradi ya Maendeleo ya Jimbo na Mkoa kwenye bajeti ya Serikali inayoendelea kujadiliwa Bungeni, Maswali na Ushauri kutoka kwa wananchama na viongozi.