Mtayarishaji wa video za muziki na filamu, Adam Juma ameeleza sababu za kusitisha kufanya video za muziki na kujikita kwenye miradi mingine ya filamu, matangazo na makala.
Mtayarishaji huyo ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Visual Lab, ameiambia Chill na Sky kuwa ingawa amekuwa akiweka juhudi kubwa katika kufanya kazi hiyo, alikutana na vikwazo vya wasanii waliokosa heshima kwenya tasnia na kazi .
Alisema kuwa pamoja na mambo mengine, alishindwa kuvumilia jinsi alivyokwazwa na wasanii wakubwa aliokubaliana nao kuwafanyia kazi tena kwa kutojali hali zao za kiuchumi kwa wakati huo lakini baadaye ‘wakamuacha kwenye mataa’ bila sababu za msingi.
“Nakumbuka niko kwenye msiba wa Ngwair, na iliniumiza sana mimi. Wiki mbili zilizopita alinitumia wimbo, na nikasema ‘hii ngoma ni kali sana, nitaifanyia kazi’. Akaniambia ‘kaka mimi sina kitu…’ nikamjibu hakuna tatizo ngoja kwanza nina mambo yangu ngoja niyamalize, nikiwa sawa tutafanya kwa sababu nataka niifanye vizuri, na heshima yako,
“Actually, wiki mbili zilizopita nilimpangia hadi siku ya kushuti, halafu baadaye hakuonekana. Baada ya siku kadhaa nikamtafuta akaniambia yuko Afrika Kusini… [nilishangaa], ‘aisee tumepanga kila kitu na ratiba halafu unaniambia umeenda Afrika Kusini’. Akaniambia ‘unajua nini, kuna vitu naweka sawa nikirudi tutaongea’. Kwakweli ile ilinikasirisha sana,” alisema.
Mtayarishaji huyo aliongeza kuwa kama hiyo haitoshi, siku kadhaa baadaye alikutana na hali kama hiyo kwa msanii Langa [Marehemu]. Hali hiyo ilimkatisha tamaa na akaamua kuachana na utayarishaji wa video za muziki na kujikita kwenye miradi mingine.
Katika hatua nyingine, Adam Juma alizungumzia uhusiano wake na Diamond Platinumz ambaye alimuandalia karibu video kumi za nyimbo zake kubwa za awali. Alisema yeye na Diamond wanaheshimiana sana, wanawasiliana na hawajawahi kuwa na ugonvi.
Hata hivyo, Adam Juma alimwaga siri ya mgogoro ulioibuka kati yake na mmoja kati ya mameneja wa Diamond Platinumz, mgogoro ambao anaamini hata Diamond mwenyewe haufahamu.
Alisema alikuwa anamdai meneja huyo kwa muda mrefu, lakini siku moja akampa fedha ambazo alimwambia ni advance ya video ya wimbo wa Diamond, lakini Adam alikata kwanza deni lake na kumwambia ajaribu kurejea kwa timu yake na kuwaeleza ukweli ili wampe fedha nyingine.
Adam Juma ni mmoja kati ya watayarishaji wa video za muziki walioiinua tasnia ya muziki wa Bongo Fleva miaka 10 iliyopita, akitumia ubunifu wake kwa teknolojia ndogo iliyokuwepo kufanya video ambazo zilipata nafasi hata kwenye tuzo kubwa za nje.