Kiungo mshambuliaji wa majogoo wa jiji Liverpool Adam Lallana amekua mchezaji wa pili kuondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England, inayoendelea na maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wa kwanza michuano ya ligi ya mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League) utakaowakutanisha na Hispania mwishoni mwa juma hili jijini London.
Lallana ameondolewa kikosini baada ya kupata majeraha ya nyonga akiwa katika mazoezi ya jana jumanne kwenye uwanja wa St George’s Park mjini Newcastle.
Kuondolewa kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30, kunakifanya kikosi cha England kusaliwa na wachezaji 22 na bado kocha mkuu Gareth Southgate, ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutoongeza mchezaji mwingine.
Mchezaji mwingine alieondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England ni mshambuliaji wa klabu bingwa nchini humo Manchester City Raheem Sterling, ambaye alibainika kuwa maumivu ya mgongo baada ya kufanyiwa vipimo juzi jumatatu.
Chama cha soka nchini England (FA), kimethibitisha taarifa za kuondoka kwa Lallana na kurejea kwenye klabu yake ya Liverpool, tayari kwa kuanza matibabu ya nyonga ambayo huenda yakamuweka nje ya uwanja kwa zaidi ya majuma mawili.
“Adam Lallana amerejea kwenye klabu yake, kwa ajili ya kuanza matibabu ya jeraha linalomsumbua,” imesomeka taarifa iliyotolewa na FA.
“Mchezaji huyo alilazimika kuondoka kambini leo (jana Jumanne), baada ya kuumia, na hatokua sehemu ya kikosi kitakachopambana na Hispania mwishoni mwa juma hili na baadae Uswiz.”
Naye kocha mkuu wa kikosi cha England Southgate, amesema hatua ya kuondoka kwa Lallana kwa sababu za kuwa majeruhi zimemuhuzunisha, lakini hana budi kukubaliana na hali halisi, na amemtakia kila la kheri katika matibabu yake.