Mshambuliaji wa pembeni wa Wolverhampton Wanderers Adama Traore ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania, licha ya kuripotiwa kukubali kuitumikia Mali, ambapo ni asili ya wazazi wake.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, ametajwa kwenye kikosi cha Hispania na taarifa zake kuthibitishwa na chama cha soka nchini Hispania (RFEF).
“Adama Traore, mchezaji wa klabu ya Wolves ya England, atajiunga na kikosi kuchukua nafasi ya Rodrigo Moreno wa Valencia, kuelekea michezo itakayotukabili siku za karibuni dhidi ya Malta na Romania,” Imeeleza taarifa iliyotolewa na RFEF.
Rodrigo Moreno aliondolewa kwennye kikosi cha Hispania, baada ya kukabiliwa na majeraha akiwa katika mchezo wa ligi dhidi ya Grananda, huku klabu yake ikiibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri, siku ya Jumamosi.
Traore ambaye ni mzaliwa na Hispania, aliwahi kuweka wazi mpango wake wa kuwa tayari kulitumikia taifa la Mali ambalo ni asili ya wazazi wake, baada kuona alikua na nafasi finyu ya kuitwa kwenye kikosi cha mabingwa wa dunia mwaka 2010.
Traore amewahi kuitumikia timu ya taifa ya Hispania chini ya umri wa miaka 21.
Msimu huu ameshaitumikia klabu yake katika michezo 10, baada ya kusajiliwa akitokea kwenye kituo cha kukuza na kulea vijana cha FC Barcelona (La Masia).
Hatua ya kuitwa kwenye kikosi cha Hispania, huenda ikamuwezesha kulitumikia taifa hilo katika timu ya wakubwa kwenye michezo ya kuwania kufuzu fainali za Ulaya (Euro 2020) dhidi ya Malta Novemba 15 na kisha Romania Novemba 18.