Nyota kutoka nchini Niger Victorien Adebayor amekiri kufurahishwa na Simba SC kuwa sehemu ya Klabu 16 zilizofuzu hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Simba SC ilitinga hatua ya Makundi ya Michuano hiyo ikizifunga Nyasa Big Bullet ya Malawi jumla ya mabao 4-0 na Primeiro De Agosto ya Angola jumla ya mabao 4-1 katika Michezo ya hatua ya awali ya Michuano hiyo.
Adebayor ambaye kwa sasa anaitumikia RS Berkane ya Morocco amesema amefurahishwa na hatua ya Wekundu hao kuendeleza kiwango chao katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na anatamani sana kuwa sehemu ya mafanikio yao.
“Kila Mchezaji anapenda kuichezea Klabu yenye kiwango kizuri katika Michuano ya Kimataifa, nimefurahishwa na hatua ya kutinga kwao Makundi,”
“Napenda kiwango cha soka na wachezaji wao, lakini kikubwa ni mzuka wa mashabiki wao wanapocheza nyumbani, inavutia sana kuona hasa wakiwa mashabiki wako.” amesema Kiungo huyo ambaye amewahi kucheza soka la Kulipwa nchini Ufaransa, Denmark na Misri kwa nyakati tofauti.
Adebayo alikaribia kutua Simba SC wakati wa Usajili wa Mwanzoni mwa msimu huu, lakini RS Berkane iliizidi kete Klabu hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kumwaga fedha nyingi za usajili, wakimtoa USGN ya Niger.
Tangu alipojiunga na RS Berkane mwanzoni mwa msimu huu, Adebayor amekua na wakati mgumu wa kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo, kama ilivyokua USGN ambapo alitegemewa sana katika safu ya ushambuliaji.