Mshambuliaji kutoka nchini Niger na klabu ya USGN Victorien Adebayor amesema mchezo dhidi ya Simba SC hakuwa na changamoto kubwa sana kwa upande wake, licha ya baadhi ya Mashabiki kuona alikua kwenye hali ngumu.
Adebayor ambaye alikua msaada mkubwa kwa USGN tangu walipopanza michuano ya kimataifa msimu huu 2021/22, amesema Simba SC ni klabu kubwa Barani Afrika na alilitambua hilo, hivyo alijiandaa kisaikolojia na alifanikiwa.
Amesema kuna wakati hakutaka kupambana kwa nguvu kwa sababu alijua Simba SC wanamtazama kama adui katika lango lao, hivyo alipambana kawaida na ndio maana alipokua akipata nafasi alizitumia kwa umakini japo hakufanikiwa.
“Ulikua mchezo mgumu sana, lakini kwangu nilijiandaa kwa kila hali kwa sababu nilijua isingekua rahisi, nashukuru hilo lilifanikiwa licha ya mambo kutuendea vibaya hadi mwishoni mwa dakika 90.”
“Sikuwa na Presha kabisa, kwa sababu nimewahi kucheza michezo migumu zaidi ya tulivyocheza hapa na Simba SC, nilijitahidi kwa kushirikiana na wenzangu na nilijaribu kutumia nafasi nilizozipata lakini sikufanikiwa na wala timu haikufanikiwa.” amesema Adebayor alipozungumza na DAr 24 Media #taarifabilamipaka.
Adebayor amemaliza michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu akiwa na amefunga mabao Sita, huku akizifunga RS Berkane na ASEC Mimosas katika michezo ya nyumbani na ugenini, lakini ameshindwa kufanya hivyo dhidi ya Simba SC.