Kocha wa zamani wa viungo wa Klabu ya Simba SC Adel Zrane ametangazwa kujiunga na Benchi la Ufundi la klabu ya Al Wehdat SC ya Nchini Jordan.
Zrane ambaye alifanya kazi kwa mapenzi makubwa Simba SC huku akijenga ukaribu na Wachezaji na Mashabiki, aliondoka Tanzania mwishoni mwa mwaka 2021, baada ya kusitishiwa mkataba wake na Uongozi.
Kocha huyo amejiunga na klabu ya Al Wehdat SC, baada ya Kocha Didier Gomez kutambulishwa klabuni hapo kama Kocha Mkuu mwishoni mwa juma lililopita.
Wawili hao walifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa wakiwa Simba SC msimu wa 2020/21, na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Kuajiriwa kwa Zrane katika klabu ya Al Wehdat SC, ni pendekezo la kocha Gomes, ambaye ameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa Mtaalamu huyo wa viungo ambaye pia aliwahi kufanya kazi na Kocha Patrick Aussems na Sven Van Den Broeck akiwa Simba SC.
Hii ni mara ya tatu kwa wawili hao kufanya kazi kwa pamoja, kwani walipoondoka Simba SC waliajiriwa kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Mauritania, kilichoshiriki AFCON 2021 nchini Cameroon.
Tetesi zinaeleza kuwa, Zrane alitarajiwa kurejea Simba SC, baada ya klabu hiyo kutangaza kuachana na Kocha wa viungo Daniel De Castro Reyes jana Jumanne (Mei 31), ambaye ameondoka sambamba na Kocha Mkuu Franco Pablo Martin.