Kocha wa Viungo kutoka nchini Tunisia na klabu ya Al Wehdat ya Jordan Adel Zraine, amesema yupo tayari kurejea Tanzania na kufanya kazi na Simba SC endapo atahitajika tena.
Zrane aliyefanya kazi kwa mafanikio makubwa Simba SC tangu alipoajiriwa mwaka 2019, ametoa kauli hiyo huku tetesi zikisema kuwa Uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi unafikiria kumrejesha kwenye Benchi la Ufundi kwa msimu ujao wa Ligi Ku na Michuano ya Kimataifa.
Akizungumza kutoka nchini Jordan, Kocha Zrane amesema anaipenda Simba SC na anaendelea kufuatilia kila kinachoendelea ndani ya klabu hiyo, hivyo hana shaka endapo atapata ofa ya kufanya kazi tena klabuni hapo.
Amesema anaamini Tanzania ni nyumbani kwake, kutokana na ukaribu aliouweka na watu wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki na wakati wote aliofanya kazi akiwa Simba SC alijihisi kama yupo nchini kwao Tunisia.
“Nipo tayari kufanya kazi tena Tanzania, najua kila kinachoendelea ndani ya Simba, ninafuatilia taarifa zao, ninafuatilia kurasa zao za mitandao ya kijamii, ninazungumza na Rafiki zangu hapo Tanzania ili kujua undani wa klabu yangu ya Simba, naipenda sana Simba SC.”
“Ikitokea Simba SC inaonyesha nia ya kufanya kazi tena na mimi sitasita kukubali ofa yao, kwa sababu ninaamini nikiwa Simba SC nitakua huru zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote ambayo nimewahi kufanya kazi katika Maisha yangu,”
Kuhusu kufanya vibaya kwa Simba SC msimu huu wa 2021/22, Zrane amesema imemuuma kusikia na kuona klabu hiyo imeshindwa kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, lakini anaamini ni shemu ya matokeo ya Soka.
Amesema Simba SC ina nafasi nyingine tena ya kurejea katika hadhi yake ya kuwa Bingwa wa Tanzania Bara kwa kutwaa mataji iliyoyapoteza msimu huu, kutokana na uhodari na utayari wa Viongozi, Wachezaji, Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo.
“Nimejisikia vibaya kuona na kusikia Simba SC imeshindwa kutetea ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, ni matokeo ya Soka, siku zote hayawezi kukubeba pekee yako, ni lazima yatawabeba na wengine,”
“Kwa namna ninavyoifahamu Simba SC, upande wa Viongozi, Wachezaji, Mashabiki na Wanachama, sina shaka kabisa kuhusu makali ya Simba SC kwa msimu ujao, Simba SC itarudi na itatisha tena katika Ligi ya hapo Tanzania na kutwaa tena mataji.” Amesema Zrane.
Zrane aliondoka Simba SC mwishoni mwa mwaka 2021 baada ya kusitishiwa mkataba wake na Uongozi, kufuatia kikosi cha Simba SC kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Kocha huyo wa Viungo alifanya kazi na makocha wote walioipa mafanikio klabu ya Simba ndani ya miaka minne, akianza na Patrick Aussems (Ubelgiji), Sven Vandenbroeck (Ubelgiji) na Didier Gomez (Ufaransa).