Aliyewahi kuwa Kocha wa Viungo wa Simba SC, Adel Zrane, amefungua milango ya kufanya kazi na miamba hiyo ya Msimbazi, endapo Uongozi wa juu utahitaji kumrudisha.
Zrane ambaye alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Simba SC ambalo lilichukua Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne mfululizo chini ya makocha Patrick Aussemns, Sven Vanderbroek na Didier Gomes.
Akizungumza kwa njia ya mtandao kutoka Rwanda, Zrane amesema kama watahitaji kufanya naye kazi hakuna shida kwa sababu anafahamu Tanzania ni kama nyumbani na Simba SC ni sehemu ya familia yake kwa kuwa aliwahi kuifundisha timu hiyo.
“Simba SC ni timu kubwa yenye malengo makubwa iwapo kama watahitaji huduma yangu ninaweza kufanya nao kazi kwani nilikuwa pale na kufanya nao kazi vizuri kwa kipindi chote na tuliishi kama familia.
“Nipo APR, ambao ndio waajiri wangu kwa sasa lakini Simba SC ni nyumbani na kama hilo jambo litaenda vizuri ninaweza kuwa sehemu ya Benchi la Ufundi ingawa ni mapema kusema lolote kwa sassa ngoja muda ufike,” amesema Zrane.
Naye Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa uongozi upo katika mchakato wa kuziba nafasi tatu kocha mkuu na msaidizi wake pamoja na kocha wa viungo na wakati wowote kuanzia leo Jumatatu (Novemba 13) ili aanze mapema maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tuna mchezo mgumu mbele yetu wa Ligi ya Mabingwa hivyo tunahitaji kuwa na Benchi la Ufundi mapema, na tayari viongozi wanaendelea na mchakato na wakati wowote tutapata mrithi wa kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho,” amesema Ahmed.