Zaidi watu 20 wameuawa katika Kijiji cha Bwanasura kilichopo jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia shambulio linalohusishwa na wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF).

Mkuu wa Idara ya usalama Kivu (KST), Mukubwa Beiza amesema shambulio hilo limetokea usiku wa kuamkia Juni 6, 2022 katika maeneo tofauti ya eneo hilo lililopo jirani na Kivu Kaskazini linalokumbwa na matukio ya uhalifu wa mara kwa mara.

“Hapa Ituli watu wanatatizika sana na mashambulizi ya makundi yenye silaha na mengi yakiwa yamerithiwa na mambo ya vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,” ameelezea Beiza.

Amesema kundi la ADF ambalo linafahamika kama Dola ya Kiislamu IS linashukiwa kuhusika na mauaji hayo na kwamba waasi wake walianza maandalizi ya mashambulio hilo June 5, 2022 majira ya saa nane mchana.

“Tumeambiwa waasi wa ADF walifika hapa karibu saa 8 mchana na wakasogea kwa utulivu ila kwa bahati nzuri wengi wa wakazi  waliwaona na waliweza kukimbia” amesema Beiza.

Awali akihojiwa na vyombo vya Habari Kiongozi wa mashirika ya kiraia wa Wilaya ya Walese Vonkutu Dieudonne Malangay, amesema Jeshi lilichelewa kufika ili kudhibiti uvamizi huo na kusema hali ya usalama bado ni tete katika eneo hilo.

Katika tukio jingine waasi wa kundi la M23 walishambulia kwa mabomu kituo cha Jeshi cha Bugusa kilichopo eneo la Rutshuru Kivu Kaskazini kisha kuwaua wanajeshi wawili na kujeruhi wengine watano.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi kupitia kwa msemaji wa Gavana Jenerali Sylvain Ekenge imeituhumu nchi ya Rwanda kuhusika na usambazaji wa silaha kwa waasi kitu ambacho kimeendeleza matukio ya uhalifu.

Mapema Mei 2022 yalizuka mapigano kati ya jeshi la DRC na kundi la M23, ambalo linadaiwa kuundwa na Watutsi wanaishi Kongo, huku mamlaka za jiji la Kinshasa DRC ikiishutumu Kigali kuwaunga mkono M23 madai ambayo yanakanushwa na nchi ya Rwanda.

Mashambulizi mbalimbali yamesababisha raia 1,300 kuuawa eneo la Irumu na Beni huko Kivu Kaskazini, 30 wakiuawa na watu wanaoshukiwa kuwa waasi wa Kivu Kaskazini na zaidi ya watu 50 walikufa katika shambulio la siku mbili katika vijiji vya Irumu.

Aidha, mapema Mei 2022 watu 42 waliuawa katika mashambulizi yanayohusishwa na kundi la ADF eneo la Bulongo na Beu-Manyama huko Kivu Kaskazini

Kundi hilo lililoanzishwa mashariki mwa DRC mwaka wa 1995, limekuwa na wafuasi wengi zaidi ambao ni wanajeshi walioachishwa kazi na kupigwa marifuku katika eneo hilo lenye machafuko.

Mwaka 2021, Marekani iliweka ADF kwenye orodha yake ya magaidi ambao wanaujamaa na mashirika ya IS, huku ikidaiwa makundi zaidi ya 120 yenye silaha yakitawala maeneo ya mashariki mwa DRC. 

Serengeti Girls wapewa nafasi za 'Mawaziri' Bungeni
TANESCO kuboresha mfumo wa manunuzi