Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi – CCM, Manispaa ya Bukoba imemtaka mkandarasi wa barabara ya Kashai, kukamilisha mradi huo mapema ili kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya usafiri.

Akizungumza katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya CCM, Mwenyekiti wa kamati hiyo Joas Zachwa amemtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi ya utendaji kazi kwani wananchi wanaotumia barabara hiyo wameteseka kwa mda mrefu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Manispaa ya Bukoba, Joas Zachwa.

Amesema “Barabara kama imefungwa ichukue mda mfupi sasa kwanini inachukua mda mrefu sana watu wanateseka, injinia swala hili uliangalie ujue kuna watu wanateseka na wanapata shida kwenye barabara hii.”

Kaimu Meneja wa Wakala wa barabara mjini na vijijini – TARURA, Injinia Keneth Dushime ameeleza sababu za kufunga barabara hiyo na kuchelewa kukamilisha ukarabati huo ni kutokana na mvua zinazonyesha mara kwa mara mkoani Kagera.

Kaimu Mkurugenzi wa TARURA, Injiania. Keneth Dushime.

“Kwa sasa tumeifunga ili tuweze kushindilia lami vizuri ili tuweze kuongeza tabaka lingine ndipo itakapokamilika, kutokana na mvua zinazoendelea hapa Bukoba tumeshindwa kumwaga tabaka la pili kwa kuwa bado kokoto hazijashindiliwa na lami haijapanda juu”. Injinia. Keneth amesema.

Nao wananchi wameeleza changamoto wanazozipata kwa sasa kutokana na ukarabati wa barabara hiyo ikiwa ni kuongezeka kwa gharama za usafiri, kuharibikiwa vyombo vya usafiri na kupata ajali.

Barabara hiyo inatengenezwa kwa kiwango cha lami urefu wa mita 100, Mkataba wake ulianza kutekelezwa Novemba 30, 2022 na ulitaraji kumalizika April 28, 2023 ikiwa unagharimu zaidi ya milioni Tsh 260.

Aishi Manula ndio basi tena Simba SC
Mawindo ya Marumo kuanza leo Kigamboni