Serikali imeonya juu ya vitendo vya unyanyasaji kwa watoto wa kike, na kuahidi kuwa itawachukulia hatua kali watu watakaowapa mimba watoto walio na umri chini ya miaka 18, wazazi wanao lazimisha kuwaoza watoto wao.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Patrobas Katambi katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike jaliyofanyika jijini Dodoma jana na kusema hawatokubali kuona binti yeyote anashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kuolewa au kupata mimba kabla ya wakati.

” Serikali ya Rais Magufuli inapiga vita vitendo vya kinyanyasaji vinavyofanywa dhidi ya mtoto wa kike hivyo jamii inatakiwa kulinda haki ya mtoto wa kike isipotee na ndani ya wilaya yangu sitaruhusu hilo litokee kamwe,” amesema Katambi.

Amesema Rais Magufuli ametoa nafasi nyingi za uongozi kwa wanawake na hiyo ni taswira kuwa jamii inatakiwa kuwa na jukumu la kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora kama maandalizi ya kuja kulitumikia Taifa katika nafasi mbalimbali kiuongozi.

Aidha Katambi pia ametumia fursa hiyo kukemea vitendo vya mila potofu kwa watoto wa kike hasa za kukubali kuwaoza wakiwa bado wanafunzi au chini ya miaka halali ya ndoa pamoja na kuwafanyia vitendo vingine vya kikatili kama vile ukeketaji na utumikishwaji kazi sehemu mbalimbali.

“Sheria zipo wazi sasa natoa onyo ukikutwa na mwanafunzi wa kike uwe ni Mwalimu, Mfanyabiashara, Mtumishi wa Serikali au bodaboda tutahakikisha tunakuchukulia hatua kali za kisheria na yeyote tutakayemkamata atakua mfano kwa wengine na ninasisitiza kuacha mila potofu,” ameongeza Mkuu huyo wa Wilaya.

Kufuatia onyo hilo pia Katambi amewataka walimu na wanafunzi kushirikiana na jamii kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria wanapobaini uwepo wa vitendo vya unyanyasaji na ukandamizaji wanavyofanyiwa watoto wa kike hasa wanafunzi na kusema ili kuwa na taifa imara lenye uchumi wa kati kupitia viwanda ni lazima pia kukubali kumnyanyua mtoto wa kike.

ALAT yaonya Ubaguzi na Rushwa Uchaguzi Serikali za Mitaa
Serikali yaagiza wafugaji kuunga mkono uhamilishaji Mifugo