Saa chache baada ya kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kutwaa ubingwa wa dunia kwa kuifunga Croatia mabao manne kwa mawili, beki wa klabu ya Olympique de Marseille Adil Rami ametangaza kustaafu kuitumikia timu hiyo.
Rami ambaye hakupata nafasi ya kucheza katika fainali za kombe la dunia za mwaka huu, ametangaza maamuzi hayo alipohojiwa na televisheni ya Ufaransa ya TF1, kwa kusema anaamini muda muafaka wa kufikia maamuzi hayo ni sasa.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 32, metangaza kuachana na timu ya taifa ya Ufaransa huku akiwa ameitumikia katika michezo 35 na kufunga bao moja, na katika fainali za mwaka 2010 alipata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Pamoja na kutokupewa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Ufaransa kilichotwaa ubingwa mwaka huu, Rami amemshukuru kocha mkuu Didier Deschamps kwa kumpa nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi kilichokwenda nchini Urusi.
“Sina budi kumshukuru kocha kwa kuonyesha namna alivyoniamini na kuniita kwenye kikosi chake, licha ya kutonipa nafasi ya kucheza katika fainali za mwaka huu, lakini naamini nilichangia baadhi ya mambo yaliyo tusababishia kutwaa ubingwa”
“Naamini kuondoka kwangu kutatoa nafasi kwa wachezaji wengine kuendelea kulitumikia taifa la Ufaransa, na ikiwezekana kuvuka mafanikio niliyoyapata tangu nilipoanza kucheza katika timu hii mwaka 2010.