Afisa Mtendaji Mkuu ‘CEO’ wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara, Adre Mtine amechimba mkwara mzito akiamini kikosi chao kina nafasi kubwa ya kutinga Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Young Africans wamepangwa kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu za Medeama ya Ghana, CR Belouizdad ya Algeria na mabingwa watetezi wa mashindano hayo Al Ahly ya Misri.
Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Young Africans kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara baada ya kupita miaka 25 tangu mara ya mwisho walivyofanya hivyo mwaka 1998 ambapo wamekata tiketi hiyo baada ya kuwaondosha Al Merrikh ya Sudan.
Mtine amefunguka kwa kujiamini baada ya baadhi ya Wadau wa Soka la Bongo kutoipa nafasi Young Africans kusonga mbele kwenye michuano hiyo, wakidai wapo katika kundi la Kifo.
Mtine amesema: “Kwanza niwaweke wazi kuwa tumeliangalia vizuri kundi letu na tunajua nini cha kufanya kufuzu Robo fainali, hatuna presha yoyote kwa kuwa tunaamini katika ubora wa kikosi chetu.
“Ni wazi kuwa hii ni hatua ngumu tunayoiendea, lakini tutapambana kuhakikisha tunafuzu hatua ya Robo fainali, inawezekana wengi hawatupi nafasi kubwa lakini sisi tunaamini tunafuzu Robo Fainali na tutawashangaza.”