Meneja wa klabu ya Sunderland, Dick Advocaat ameweka wazi mustakabali wake ndani ya klabu hiyo baada ya mambo kumuendea ndivyo sivyo tangu mwanzoni mwa msimu huu kwa kushuhudia kikosi chake kikishindwa kupata ushindi katika michezo sita waliyocheza mpaka sasa.

Advocaat ambaye alikinusuru kikosi cha Sunderland kushuka daraja mwishoni mwa msimu uliopita na kuondoka klabuni hapo kabla ya kurejea miezi mitatu iliyopita, amesema atakua tayari kurejea nyumbani kwao Uholanzi na kuendelea na maisha endapo viongozi watamtaka kufanya hivyo.

Amesema anaona alipofika kwa sasa anahitaji usaidizi wa mtu mwingine, ambaye ataonekana anafaa kukiendesha kikosi cha The Black Cats, na atakapopewa taarifa za ujio wa mtu huyo atakuwa radhi kuondoka na kumuachia majukumu.

Meneja huyo ambaye aliwahi kuvinoa vilabu vikubwa duniani kama PSV, AZ Alkmaar pamoja na Rangers amesisitiza jambo hilo baada ya kuona vyombo vya habari vimeanza kumuandama kwa kueleza hafai kuendelea kuwa meneja wa klabu ya Sunderland.

Mbali na kuvinoa vilabu, pia Advocaat amewahi kuwa kocha mkuu wa timu za mataifa mbali mbali dunia kama Korea Kusini, Urusi, Uholanzi, Serbia pamoja na Ubelgiji.

Sunderland imekua na bahati mbaya ya kubadili mameneja zaidi ya wawili kwa misimu miwili sasa hali aambayo imekua ikitajwa kama sababu ya wachezaji kushindwa kufuata maelekezo ya makocha kwa wakati mmoja na hatimaye hujikuta wakipoteza muelekeo wa ushindani.

Mameneja waliowahi kupita klabu hapo kwa miaka ya hivi karibuni na wameshindwa kufikia malengo ni Gus Poyet, Kevin Ball, Paolo Di Canio, Martin O’Neill, Eric Black pamoja na Steve Bruce.

Malinzi Afunga Kozi Ya Makocha Leseni C
Soka la Wanawake Kuanza Kutimua Vumbi Mikoani