Nguli wa Bongo Fleva, Selemani ‘Afande Sele’ Msindi amesema kuwa anajipanga kumuondoa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi kwenye kiti cha ubunge mwaka 2020.
Afande ambaye hivi sasa ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyekabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa chama hicho, Dkt. John Magufuli alipoimwaga ACT-Wazalendo, amesema amechukua uamuzi huo baada ya kuona kuwa Sugu hajaleta maendeleo yoyote Mbeya bali amejineemesha.
“Sasa hivi ana miaka kumi [jimboni] lakini inaonekana yeye hata kwenye nyimbo zake unaweza kumsikia anavyoimba, anajisifu yeye haisifii Mbeya. Kwamba ana hoteli kubwa ya kisasa, kwamba ana marafiki wakubwa akina Chenge na matajiri wakubwa… Kwahiyo haizungumzii Mbeya aliyeiomba kama ataisaidia,” Sugu aliiambia Clouds Media.
Alisema atahakikisha mwaka 2020 anampigia debe mgombea wa CCM atakayegombea katika jimbo hilo na kuhakikisha jimbo linarudi kwenye chama hicho tawala.
Aidha, Afande amenuia kumng’oa pia mwanamuziki mwenzake, swahiba waliyeshirikiana naye kwenye wimbo mkubwa wa muda wote ‘Mtazamo’, Mbunge wa Mikumi, Joseph ‘Profesa Jay’ Haule.
Amesema kuwa ingawa yeye ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kumtangaza na kumtambulisha Profesa Jay kwa wananchi wa Mikumi, haoni maendeleo aliyowaletea wananchi wa jimbo hilo bali amejineemesha kwa kujenga shule ya kisasa jijini Dar es Salaam.
“Kwahiyo nitawapigia debe wagombea wangu wa chama tawala ili waweze kuingia madarakani kuweza kutekeleza sera na ilani ya CCM ambayo naamini itawafanya vijana na akina mama wa Mbeya [na Mikumi], wabadilishe maisha yao kwa muda mfupi kwa kiasi fulani,” alisema.
Afande Sele ambaye aliwahi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Morogoro amedai kuwa angekuwa yeye ndiye aliyeko kwenye nafasi ya wanamuziki hao walioingia bungeni, angetumia nafasi yake kuwatafutia mikopo ya bei rahisi akina mama na vijana pamoja na kujenga shule.
Afande ni mmoja kati ya wasanii wakongwe wenye ushawishi kwa mashabiki wake, akiwa na heshima ya Ufalme wa Rhymes alioupata kupitia mashindano pekee ya wanamuziki wote wa Bongo Fleva kuwahi kufanyika nchini.
Je, Nguli huyu ataweza kumng’oa Sugu Mbeya kwa kuzingatia historia kuwa Sugu ndiye mbunge aliyepata kura nyingi zaidi katika uchaguzi uliopita?