Rapa Mkongwe, Selemani ‘Afande Sele’ Msindi ambaye ndiye rapa pekee aliyetunukiwa taji la ‘Ufalme wa Rhymes’ takribani muongo mmoja uliopita na kugeuka kuwa Mfalme Selemani, amesema kuwa sikio lake halijakunwa na rapa yeyote kiasi cha kumpa vigezo vya kumrithisha taji hilo.

Akiongea na Ladha 3600 ya E-FM, Afande Sele amesema kuwa msanii mwenye uwezo kama yeye bado hajazaliwa chini ya ardhi ya Tanzania, hivyo haoni mbadala wowote wa kipaji chake.

“Mtu anayeweza kufanya kazi kama yangu hajazaliwa bado. Labda aje mfalme feki au ambaye alijipa. Lakini mimi nilipewa na watu, nilipigiwa kura na nikachaguliwa mbele za watu,” Afande Sele alimwambia Jabir Saleh, mtangazaji wa kipindi hicho.

Alisema kuwa hata baadhi ya wasanii wa zamani ambao hivi sasa wako kimya hawaulizwi na mashabiki ujio wao mpya wala kuwaomba watoe ngoma, tofauti na yeye ambaye hata akiandika ujumbe kwenye Facebook hupokea maombi mengi ya mashabiki wakitaka kumsikia tena.

Rapa huyo mkongwe ambaye mwaka jana alijitosa kwenye siasa kuwania ubunge Mjini Morogoro amesema kuwa wasanii wa sasa hawaumizi kichwa kufanya kazi kubwa na ya kipekee kama aliyofanya yeye.

“Watu hawataki kufikiri, hawataki kuumiza kichwa. Utakuta mtu pengine ana GB 10 kwenye ubongo wake lakini anataka kutumia GB 1 tu maisha yake yote, zile zingine hajazitumia kwa sababu hataki kuumiza kichwa,” alisema Afande.

Afande Sele alishinda kuwa Mfalme wa Rhymes katika shindano moja kubwa lililowakutanisha jukwaani wasanii kumi wakubwa waliopita kwenye mchujo wa kupigiwa kura na wananchi kupitia gazeti moja pendwa wakati huo.

Wimbo wake ‘Darubini Kali’ ulikuwa fimbo nzito iliyompa nafasi zaidi katika mashindano hayo yaliyoweka historia kubwa kuwahi kutokea kwenye muziki wa Bongo Flava katika jukwaa moja.

Mashambulizi ya Kituo cha Polisi Kapenguria Bado Sintofahamu
Rwanda Yagomea Ombi la ICC Kumkamata Bashir