Mwanafunzi mmoja wa mwaka wa kwanza katika chuo kikuu cha Maasai Mara nchini Kenya, ameripotiwa kufariki siku ya Alhamisi baada ya uume wake kudaiwa kusimama kwa muda mrefu.
Taarifa za polisi nchini humo zinasema, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21 alifariki katika hospitali ya Shepherd ambako alilazwa asubuhi ya Jumatano baada ya kulalamika kuhusu maumivu tumboni na uume wake kusimama kwa muda mrefu bila kupoa.
Ripoti hiyo inasema kwamba uchunguzi wa awali umebaini kuwa uume wa marehemu ulianza kusimama punde baada ya kula chakula katika sherehe ambayo alikuwa amehudhuria Jumamosi na wanafunzi wenzake watano.
Hali hiyo iliendelea kwa siku tatu hadi Jumatatu ambapo alichuku maamuzi ya kutembelea zahanati ya shule hiyo kwa matibabu na alipokea matibabu na kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Hata hivyo marehemu alipelekwa katika hospitali ya Shepherd siku ya Jumatano ambako alifariki.
Polisi wameripoti kuwa mkuu wa shule hiyo aliandikisha taarifa kuhusu kifo cha mwanafunzi huyo saa kumi alasiri ya Alhamisi.