Mwanaume mmoja nchini Kenya aliyedhaniwa amefariki dunia na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti na “kupata tena fahamu” wiki iliyopita, Peter Kigen, sasa amefariki kweli, kwa mujibu wa vyombo vya habari katika eneo hilo.

Taarifa zinadai wiki iliyopita muhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti alikuwa akitayarisha mwili wa Kigen ili kuuweka kwenye chumba maalum kwa ajili ya wafu, kabla ya mwanaume huyo kupata fahamu ghafla na kuanza kupiga kelele.

Kigen, 32, ambaye alikuwa ameugua kwa muda mrefu, alipekwa hospitali kupata matibabu na baadaye, akaruhusiwa kwenda nyumbani ambapo Alhamisi iliyopita alizungumza na gazeti la Kenya la Daily Nation, na kueleza kuwa ni mwenye furaha kuwa hai kwani hiyo ni kazi ya Mungu.

Tukio hilo lilisabisha wengi kutoa maoni yao katika mitandao ya kijamii, na pia likajadiliwa katika bunge la kaunti ya Kericho ambalo liliamua kuunda timu kuchunguza kile hasa kilichotokea, taarifa ambayo iliwaondolea wahudumu wa afya lawama.

Jana Alhamisi, msemaji wa familia alithibitisha kifo cha kweli cha mwanaume huyo kupitia gazeti la Standard la nchini Kenya.

“Kigen alitangazwa kufariki dunia baada ya kufika hospitali ya kaunti ya Kericho alikopelekwa kutoka hospitali ya Kapkatet kwa matibabu zaidi,” amesema Hezbon Tonui .

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Desemba 5, 2020
Gattuso kusaini mkataba mpya SSC Napoli