Klabu ya Bournemouth imemsajili moja kwa moja beki Nathan Ake, baada ya kumtumia kwa mkopo akitokea kwa mabingwa wa soka nchini England Chelsea.
Beki huyo kutoka nchini Uholanzi, aliitumikia AFC Bournemouth kwa mkopo msimu uliopita na alifanikiwa kufunga mabao matatu katika michezo 12 aliyocheza.
Ake mwenye umri wa miaka 22, amekamilisha mpango wa kuondoka moja kwa moja Stamford Bridge kwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 20, ambayo inavunja rekodi ya usajili ya AFC Bournemouth.
Kwa mara ya mwisho AFC Bournemouth ilimsajili mshambuliaji wa pembeni Jordon Ibe kwa Pauni milioni 15, alipoihama Liverpool Julai 2016.
Ake amesaini mkataba wa muda mrefu, na anakua mchezaji watatu kusajiliwa na FC Bournemouth, akitanguliwa na mshambuliaji Jermain Defoe aliyetokea Sunderland na mlinda mlango kutoka Bosnia Asmir Begovic aliyekua mali ya Chelsea.