Kocha Mkuu wa Dodoma jiji FC Melis Medo anahusishwa na mpango wa kuwindwa na Klabu ya AFC Leopards inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka nchini Kenya,  kufuatia timu hiyo kuwa na matokeo yasiyoridhisha.

Medo anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Patrick Aussems ‘Uchebe’ baada ya mabosi wa AFC Leopards kutofurahishwa na mwenendo wake, msimu huu 2022/23.

Taarifa kutoka jijini Nairobi zinaeleza kuwa, kocha huyo yupo kwenye mazungumzo ya karibu na mabosi wa AFC Leopards kwani si mara ya kwanza kuhitaji huduma yake na ilishawahi kutokea wakati akifundisha nchini humo kwenye klabu ya Wazito.

Inadaiwa kuwa kutokana na ukaribu wake na Kocha msaidizi wa Dodoma Jiji, wawili hao kama watakubaliana vizuri na mabosi wa Leopards wanaweza kuondoka pamoja.

Kwa sasa, AFC Leopards ipo katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Kenya ikicheza mechi 31, huku ikijikusanyia alama 48.

Mtu wa karibu na kocha huyo alipotafutwa amesema: “Kweli kuna hizo taarifa baada ya mitandao mingi ya Kenya kuandika, lakini kwa sasa kocha anaangalia zaidi kumaliza mechi za hapa.”

Alipotafutwa katibu mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson amesema ni habari ngeni kwake kwa sababu wasingeweza kutafutwa wao bali ni muhusika lakini watahakikisha kocha wao haondoki.

“Hizi taarifa ndio naziona hapa lakini sisi makocha wetu wanamaliza mikataba na tupo kwenye mazungumzo nao, tukielewana tutaendelea nao lakini tukishindwana hakuna namna,”amesema Fortunatus

Dodoma Jiji kwa sasa inashika nafasi ya 11 ikiwa na alama 31 kwenye mechi 28 ilizocheza.

Wizara ya Nishati yataja vipaumbele bajeti 2023/2024
Kilio cha Wananchi Kilolo: Chongolo atoa siku 10 kwa Waziri