Matokeo ya sare ya mabao mawili kwa mawili yameshindwa kuivusha timu ya taifa ya Algeria katika hatua ya makundi, na sasa imeondoshwa kwenye fainali za Afrika (AFCON 2017).
Algeria ambao walipewa nafasi ya kuleta ushindani mkubwa katika fainali za mwaka huu, na wengine waliamini huenda wangekua mabingwa wa Afrika, walilazimishwa sare na timu ya taifa ya Senegal katika mchezo wa mwisho wa kundi B.
Hata hivyo Algeria walikua wa kwanza kupata bao katika dakika ya 10 kupitia kwa Islam Slimani, lakini Senegal walifanikiwa kusawazisha dakika ya 44 kupitia kwa Pape Kouli Diop, lakini Islam Slimani aliifungia bao la pili dakika ya 52 kabla ya Moussa Sow kusawazisha dakika ya 54 na kuufanya mchezo kumalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili.
Mchezo mwingine wa kundi B ulishuhudia kikosi cha Tunisia kikipapatuana na Zimbabwe ambao walikubali kufungwa mabao manne kwa mawili.
Mabao ya Tunisia yalifungwa na Naim Sliti, Yousesf Msakni, Taha Yassine Khenissi na Wahbi Khazri dakika ya 9, 22, 36, 45 huku mabao ya Zimbabwe yakipachikwa wavuni na Knowledge Musona na Tendai Ndoro dakika ya 43 na 58.
Matokeo hayo ya michezo ya mwisho ya kundi B, yanaipa nafasi Senegal kuongoza kwa kufkisha point 7, wakifuatiwa na Senegal wenye point 6, Algeria point 2 na Zimbabwe wanaburuza mkia kwa kuwa na point 1.
Michuano hiyo inaendelea tena hii leo kwa michezo ya mwisho ya kundui C, ambapo mabingwa watetezi Ivory Coast watapambana na Morocco huku Togo watachuana na Congo DRC.
Msimamo wa kundi hilo Congo DRC wanaongoza kwa kufikisha point 4, wakifuatiwa na Morocco wenye point 3, Ivory Coast ni wa tatu kwa kufikisha point 2 na Togo wanaburuza mkia kwa kupata point moja.