Wenyeji wa fainali za Afrika (AFCON 2017) timu ya taifa ya Gabon, wametupwa nje ya michuano hiyo katika hatua ya makundi, baada ya kuambulia matokeo ya sare katika mchezo dhidi ya Cameroon.
Gabon, walipaswa kupata ushindi katika mchezo huo ili kujiweka katika mazingira ya ushindani wa kusonga kwenye hatua ya robo fainali dhidi ya Burkina Faso, lakini ilikua tofauti namatarajio ya walio wengi.
Matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Cameroon, yameifanya Gabon kufikisha point tatu, ambazo zinawaweka kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi A.
Hata hivyo wenyeji hao wanaondoka kwenye michuano hiyo, huku wakiwa na kumbukumbu ya kutopoteza mchezo hata mmoja, na badala yake wameambulia sare.
Wakati Gabon wakisukumwa nje ya michuano hiyo, Burkina Faso walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Guinea Bissau.
Rudinilson Silva alijifunga katika dakika ya 12 na Bertrand Traore aliongeza bao la pili dakika ya 58.
Kwa matokeo hayo Burkina Faso wanaongoza msimamo wa kundi A kwa kufikisha point tano sawa na Cameroon, lakini wana faida ya uwiyano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika hatua ya makundi Burkina Faso wamefunga mabao manne na kufungwa mabao mawili, huku Cameroon wakifunga mabao matatu na kufungwa mawili.
Hii leo michuano hiyo itashuhudia michezo ya mwisho ya kundi B, ambapo Senegal watapambana na Algeria ilhali Zimbabwe watapapatuana na Tunisia.
Michezo yote itachezwa saa nne kamili usiku, kwa saa za Afrika mashariki.