Mabao yaliyofungwa na Junior Kabananga, Firmin Mubele Ndombe na Paul-Jose M’Poku yalitosha kuhitimisha safari ya timu ya taifa ya Congo DRC kutinga hatua ya robo fainali ya michuano Afrika (AFCON 2017) wakitokea katika kundi C.
Mabao hayo yaliofungwa katika dakika 29, 54 na 80 dhidi ya Togo, yaliiwezesha congo DRC kufikisha point saba na kuongoza kundi hilo na sasa wanamsubiri mshindi wa pili wa kundi D ambaye atajulikana hii leo.
Hata hivyo Togo hawakutoka uwanjani mikono mitupu, bali walipata bao moja la kufutia machozi lililofungwa na Kodjo Laba Fodoh katika dakika ya 69 na kuufanya ubao wa magoli kusomeka tatu moja.
Togo iliyokua inaongozwa na mshambuliaji ambaye hana klabu kwa sasa Emmanuel Adebayor, imetupwa nje ya michuano hiyo, baada ya kupoteza michezo miwili na kujikuta wakimaliza michezo ya hatua ya makundi wakiwa na point moja.
Katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Togo walilazimisha matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Ivory Coast.