Kocha wa mabingwa wa Afrika mwaka 2017 timu ya taifa ya Cameroon Hugo Broos, amewashukuru wachezaji wake 23 aliokwenda nao kwenye michuano ya AFCON iliyomalizika nchini Gabon siku ya jumapili.
Broos ambaye alikua hapewi nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika fainali za AFCON za mwaka huu, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, wachezaji wote 23 aliokwenda nao nchini Gabon walichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio aliyoyapata.
Alisema angekua mchoyo wa fadhila kama angeshindwa kuwashukuru wote kwa ujumla, kutokana na kutambua umuhimu wa kila mmoja, kwani anaamini ushirikiano wao mkubwa waliouonyesha wakiwa kambini, mazoezini na hata katika viwanja walivyoshindana, ulikua chachu ya mazuri waliyoyavuna.
Hata hivyo kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji, aliwathibitishia wachezaji aliokwenda nao nchini Gabon kwa kuwaambia wataendelea kuwa sehemu ya kikosi chake katika michuano mingine itakayowakabili siku za usoni, huku akisisitiza kuongeza damu changa.
Cameroon walitwaa ubingwa wa Afrika siku ya jumapili kwa kuichapa Misri mabao mawili kwa moja, na kufanikisha furaha yao ya kuwa mabingwa wa Afrika kwa mara ya tano.
Mabao ya Cameroon katika mchezo huo yalifungwa na Nicolas Nkoulou pamoja na Vincent Aboubakar huku Mohamed Elneny akipachika bao pekee la Misri katika mpambano huo uliounguruma mjini Libreville.
Kwa mafanikio hayo Cameroon watakua wawakilishi wa bara la Afrika katika fainali za kombe la mabara, ambazo zitachezwa nchini Urusi mwezi Juni mwaka huu.