Mshambuliaji wa klabu ya AS Roma ya nchini Italia Mohamed Salah, ameiwezesha timu ya taifa lake la Misri kutinga katika hatua ya robo fainali ya michuano ya mataifa ya Afrika mwaka 2017 (AFCON 2017) inayoendelea nchini Gabon.
Misri walicheza mchezo wa mwisho wa kundi D dhidi ya Ghana, ambao tayari walikua wameshajihakikishia nafasi ya kusonga mbele kabla ya mchezo huo, kufuatia ushindi walioupata kwenye michezo miwili ya awali.
Salah alifunga bao hilo pekee na la ushindi kwa Misri, baada ya kupiga mkwaju wa adhabu ndogo ambao ulikwenda moja kwa moja langoni mwa Ghana katika dakika ya 11.
Ushindi huo unaibeba Misri hadi katika nafasi ya kwanza katika msimamo wa kundi D, kwa kufikisha point 7, zinazotokana na ushindi kwenye michezo miwili na sare moja.
Kwa mantiki hiyo sasa Misri watacheza dhidi ya Morocco kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali, huku Ghana waliomaliza kwenye nafasi ya pili ya kundi D wakiwasubiri DRC Congo.