Mwamuzi kutoka nchini Gambia Papa Bakary Gassama amepewa jukumu la kupuliza kipyenga katika mchezo wa nusu fainali ya pili ya michuano ya Afrika, kati ya Cameroon na Ghana.

Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 38, alitajwa kuwa mwamuzi bora wa mwaka katika hafla za utoaji wa tuzo za walio bora kwa mwaka 2016, zilizofanyika mjini Abuja nchini Nigeria mwanzoni mwa mwaka huu, chini ya usimamizi wa shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Hii ni mara ya tatu kwa Gassama kutangazwa kuwa mwamuzi bora wa Afrika wa mwaka, na inatarajiwa atafanya kazi nzuri katika majukumu yake ya kusimamia sheria 17 za mchezo wa soka hii leo.

Kwa mara ya mwisho alichezesha mchezo uliyoihusu Ghana wakati wa hatua ya makundi, ambapo The Black Stars walikubali kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Misri.

Mwaka 2015 pia alichezesha mchezo uliyoihusu timu hiyo kutoka Afrika magharibi, ambapo Ghana walipoteza mchezo wa fainali dhidi ya Ivory Coast kwa changamoto ya mikwaju ya penati.

Mchezo wa leo wa nusu fainali utaendelea kumpa heshima mwamuzi huyo mwenye beji ya FIFA, na tayari ameshachezesha michezo 12 ya AFCON tangu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2012.

Video: Siri ya rais Magufuli kukutana na marais wa Afrika Mjini Addis Ababa
AFCON 2017: Asamoah Gyan Aibua Matumaini