Kabla ya kuikabili na Sudan katika mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki, Kiungo Mshambuliaji wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Simon Msuva, amesema motisha ya fedha walizopata kutoka kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, zimewapa nguvu zaidi ya kujituma uwanjani.
Taifa Stars itacheza wa mchezo huo wa Kirafiki dhidi ya Sudan ambao utafanyikia Saudi Arabia.
Msuva amesema ni faraja kwao kuona Rais Dk. Samia anawasapoti katika kazi yao, hivyo inawapa moyo wa kufanya vizuri zaidi.
“Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia, hii inatusaidia sisi kujiona kama tuna deni hivyo tunapambana tunapokuwa uwanjani, tutafanya vizuri dhidi ya Sudan kumfurahisha,” amesema.
Msuva amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo, wanaamini kikosi alichokiita Kocha Adel Amrouche, kitashirikiana kuhakikisha wanarudi na furaha.
Stars inacheza mchezo huo kujiandaa na michuano ya AFCON ambayo imepangwa kufanyika mwakani nchini lvory Coast, huku Tanzania ikipangwa Kundi F lenye timu za Zambia, Morocco na DR Congo.
Baada ya Tanzania kufuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) zitakakofanyika Januari mwakani, DK. Samia alitoa kiasi cha sh. milioni 500 ikiwa ni motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Kikosi ambacho kinakwenda kuivaa Sudan kinaundwa na Beno Kakolanya, (Singida FG), Metacha Mnata, Nickson Kibabage, lbrahim Hamad, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Mudathir Yahya na Clement Mzize wote wa Young Africans.
Kutoka kikosi cha Simba wamo Aly Salim, Israel Mwenda, Kibu Denis na Mzamiru Yassin, Abdul Suleiman na Sospeter Bajana wa Azam FC, Nassor Saadun (Ihefu FC) na Abdulmalik Zakaria (NaeKabvlie-Algeria). (Namungo FC).
Wengine ni Msuva (JS Soura -Algeria), Abdulrazak Hamza (Super Sport-Afrika Kusini), Baraka Majokoro (Chippa United-Afrika Kusini), George Mpole (Saint loi Lupopo-Congo DR), Said Hamis na Morice Abraham wote kutoka FKJedinstvo ya Serbia).
Wamo pia Haji Mnoga (Andershot Town-Uingereza), Ben Starkie (Basford United-Uingereza), Novatus Miroshi (Shakhtar Donetsk-Ukraine), Mbwana Samatta (Paok FC-Ugiriki), Abdi Banda (Richards Bay FC-Afrika Kusini) na Himid Mao (Tala’ea El Gaish-Misri).