Timu ya taifa ya Senegal imekua ya kwanza kutinga katika hatau ya robo fainali ya michuano ya Afrika (AFCON 2017) inayoendelea nchini Gabon.
Senegal wamefikisha point sita, baada ya kuifunga timu ya taifa ya Zimbabwe mabao mawili kwa sifuri usiku wa kuamkia hii leo, huku ikikumbukwa katika mchezo wao wa kwanza wa kundi B waliifunga Tunisia mabao mawili kwa sifuri.
Mabao ya Senegal katika mchezo dhidi ya Zimbabwe yalikwamishwa wavuni na Sadio Mane na Henri Saivet katika dakika ya 9 na 14.
Pamoja na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali, Senegal bado wanakabiliwa na mchezo mmoja wa hatua ya makundi dhidi ya Algeria ambao utachezwa Januari 23.
Kabla ya mpambano wa Zimbabwe na Senegal ambao ulichezwa kuanzia saa nne usiku kwa saa za Afrika mashariki, mahasimu wawili kutoka Afrika ya Kaskazini Tunisia na Algeria walipapatuana.
Tunisia walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja, ambapo katika dakika ya 50 beki wa kulia wa klabu ya Real Betis Aissa Mandi alijifunga na dakika 16 baadae, kiungo mshambuliaji wa klabu ya Red Star ya Ufaransa, aliifungia Tunisia bao la pili na la ushindi.
Matokeo hayo yanaiweka pabaya Algeria katika harakati za kusonga mbele kwenye fainali za Afrika za mwaka huu, na kama watahitaji kufaulu mtihani huo, watalazimika kuifunga Senegal kwa idadi kubwa ya mabao.
Michuano hiyo inaendelea tena hii leo kwa michezo ya kundi C, ambapo mabingwa watetezi Ivory Coast watapambana na kikosi cha Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo mishale ya saa moja jioni kwa saa za Afrika mashariki na baadae saa nne usiku Morocco watacheza dhidi ya Togo.